Kwanini migogoro ya ndoa inaongezeka badala ya Kupungua? Soma hapa ujue!
Migogoro ya kifamilia ni changamoto kubwa na hutokea pale mwanafamilia anapokuwa na mtazamo tofauti wa mawazo na mwanafamilia mwingine. Mara nyingi migogoro ya familia hutokea kwa misuguano midogo na kukimbilia katika uamuzi usiofaa.
Kukwaruzana kusiposhughulikiwa kwa muda muafaka husababisha migogoro na mifarakano mbalimbali ndani ya familia. Kuna njia mbalimbali za mawasiliano zinazolenga kurejesha amani na upendo ndani ya familia. Njia hizo ni makubaliano ya pamoja au kukubali kwa kutokukubaliana.
Kwa nini migogoro ya kifamilia inazidi badala ya kupungua?Zipo sababu nyingi zinazochangia kuongezeka kwa migogoro ya familia. Baadhi ya sababu hizo ni:
Kuishi katika nchi maskini. Umasikini wa nchi hasa wa kipato ukitafsiriwa katika ngazi ya familia uonekane mkubwa kwani mahitaji muhimu (chakula, mavazi, hifadhi) huongezeka na kipato ndani ya familia hupungua.
Hali hii huchangia kwa wanafamilia kutokuelewana kwa sababu ya maisha magumu kila siku na wakati huo huo pengo la familia za walionacho na wasionacho likizidi kuongezeka.
Ongezeko la familia. Hali ya kujifunza kuishi kifamilia, kuzaliwa kwa watoto, kuongezeka kwa mahitaji na matumizi muhimu ya kifamilia ni sababu nyingine inayochangia kuongezeka kwa migogoro ya familia.
Ukosefu wa uaminifu. Kukosekana kwa uaminifu mara nyingi huwa ni chanzo cha mifarakano ya kifamilia katika jamii. Matumizi ya maneno yanayojenga uhusiano mwema ndani ya familia kama vile; ‘niamini’, ‘nakupenda’, nisamehe, nivumilie na mengine mengi kama hayo.
Maneno hayo husaidia kudumisha amani na upendo katika familia. Ukosefu wa uaminifu huharibu uhusiano, uwajibikaji na mbaya zaidi husababisha kutoaminiana miongoni mwa wanafamilia.
Ufahamu mdogo wa maisha ya familia. Uhusiano wa kifamilia ni changamoto kwa kila mtu bila kujali jinsia, kipato, au kiwango cha elimu. Hivyo inatakiwa kusoma vitini vya uhusiano na kuomba ushauri kwa wenzetu wenye uzoefu zaidi katika masuala ya kifamilia. Kwa mfano, wanafamilia wachanga wanashauriwa kutumia wazee katika masuala ya ndoa na malezi ya familia.
Uelewa mdogo, kukaa sehemu moja, hasira, jazba, matumizi ya nguvu, ulevi kupindukia, talaka, ulafi, vipigo, kutelekeza familia, kutumia muda mwingi kazini, na mengine mengi ambayo hatutakiwi kudharau ili kujenga familia imara na zenye mahusiano mema.

Comments
Post a Comment